BARABARA YA MPEMBA

 
BARABARA YA MPEMBA-ISONGOLE KM 58 KUJENGWA KWA KIWANGO CHA LAMI
 
Waziri wa Ujenzi Dkt. John Pombe Magufuli amekagua barabara ya Mpemba-Isongole yenye urefu wa km 58 Wilayani Ileje na kuahidi kuwa Serikali itaijenga kwa kiwango cha lami.
 
Akizungumza mara baada ya kufungua sehemu ya barabara ya lami wilayani humo kati ya Isongole hadi Itumba km 9, Waziri Magufuli amesema Serikali itaijenga kwa kiwango cha lami barabara ya Mpemba-Itumba km 58, ili kufungua fursa za uchumi wilayani Ileje na kuhakikisha barabara hiyo inaungana na nchi ya Malawi kwa kiwango cha lami.
“Barabara ya lami ni muhimu kujengwa katika Wilaya ya Ileje ili kukuza uchumi wa wananchi ambao wana mazao mengi yanayohitaji usafiri wa uhakika kufikia masoko”, amefafanua Dkt. Magufuli.
 
Waziri Magufuli amezungumzia umuhimu wa kuiunganisha Wilaya ya Ileje na mtandao wa barabara unaoanzia Bukoba –Biharamulo- Uvinza-Mpanda-Sumbawanga-Tunduma-Mpemba-Isongole hadi Chitipa nchini Malawi ambapo ikikamilika kwa lami itafungua ukanda muhimu wa biashara na kukuza uchumi wa nchi.
 
Amehimiza umuhimu wa Wilaya ya Ileje kutumia fedha za mfuko wa barabara kujenga barabara za lami ili kurahisisha huduma za usafiri na kuvutia wataalam wengi kufanyakazi na kuishi wilayani humo.
 
“Hakikisheni mnafanyakazi kwa umoja na mshikamano kwa kuepuka majungu na rushwa ili mfikie malengo na mwaka huu tutawapa shilingi milioni 721 kwaajili ya barabara”, amesisitiza Waziri Magufuli.
 
Awali, alipokuwa anakagua Mzani wa Mpemba, Waziri Magufuli aliwahimiza wafanyakazi wa Mzani huo kufanyakazi kwa weledi na uadilifu na hivyo kujiepusha na vitendo vya rushwa ili kutenda haki kwa wasafirishaji.
 
Naye, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Eng. Musa Iyombe amesema barabara ya Mpemba hadi Isongole itakayojengwa kwa kiwango cha lami ilikuwa barabara ya Wilaya lakini kutokana na umuhimu wake Serikali imeipandisha hadhi kuwa ya mkoa na tayari upembuzi yakinifu kuhusu ujenzi wa barabara hiyo umekamilika.
 
Kwa upande wa Mkuu wa wilaya ya Ileje Rosemary Sinyamule amemhakikishia Waziri Magufuli kuwa Wilaya hiyo ina upungufu wa barabara za lami hivyo ujenzi wake utavutia watumishi kuishi na kufanya kazi katika wilaya hiyo inayopakana na nchi za Malawi na Zambia.