Makandarasi wameaswa kufanya kazi kwa viwango na ubora unaotakiwa kwa kuzingatia makubaliano katika mikataba ya utekelezaji wa miradi.
Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo ya Usimamizi wa Mikataba (Contracts Management) ya siku tatu yaliyofanyika kuanzia tarehe 07 Julai hadi 01 Agosti, 2025 yenye lengo la kuwajengea uwezo Makandarasi wazawa yaliyofanyika Mkoani Iringa, Msajili wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), Mhandisi Rhoben Nkori, amesema kuwa lengo la kufanya mafunzo hayo ni kutoa elimu kwa Makandarasi na kuwakumbusha umuhimu wa kuzingatia wajibu wao pamoja na haki zao kama zinavyoainishwa katika mikataba ya kazi zao.
“Kupitia mafunzo yatakayotolewa naamini mtajifunza mada mbalimbali ikiwemo kuzijua na kuzingatia haki na wajibu wenu kwa kuzingatia mikataba ya miradi mbalimbali mnayotekeleza”, alisema Mhandisi Nkori.
Mhandisi Nkori aliongezea kuwa, ukandarasi ni biashara ya kimkataba hivyo ni wajibu wa kila Mkandarasi kuwa na ujuzi wa usimamizi wa mikataba ili kujua haki zake na kutekeleza wajibu wake ipasavyo na kuepuka kufanya biashara hiyo kwa upendeleo au kwa maslahi bianfsi bali wazingatie maadili ya taaluma zao.
"Biashara ya ukandarasi ni ya kitaalamu, lakini wapo baadhi ya Makandarasi wamekuwa wakiiendesha kinyume na misingi ya taaluma. Mkandarasi unapoingia mkataba, haijalishi unafahamiana na nani unatakiwa kutekeleza wajibu wako ipasavyo ili kuepuka kuchukuliwa hatua za kisheria," alisema Mhandisi Nkori.
Aidha Mhandisi Nkori, alitoa rai kwa Makandarasi kuzichangamkia fursa mbalimbali za mafunzo yanayoandaliwa na Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) ndani na nje ya nchi kwa ajili ya kujifunza kwa vitendo ili kujengewa uwezo mzuri utakaowasaidia wakati wa utendaji wa kazi zao.
Mafunzo haya yamewakutanisha washiriki zaidi ya 100 kutoka mikoa 10 hapa nchini wakiwemo Makandarasi na Waajiri
Photo by:Admin, 2025-08-13 06:06:09 |
Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amesema kuanzia sasa miradi yote ya ujenzi ambayo thamani yake haizidi shilingi bilioni 50 kipaumbele kitakuwa ni wakandarasi wazawa.
Akizungumza katika mkutano na wakandarasi wazawa uliofanyika Dodoma leo, Ulega alisema uamuzi huo unatokana na maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan kutaka wakandarasi wazawa wapewe miradi mingi ya ujenzi ili wakue na kukuza uwezo wa kufanya miradi mikubwa zaidi.
Katika kuonyesha dhamira ya dhati ya serikali katika kutimiza azma hiyo, Ulega amesema Serikali imeingia mikataba ya takriban shilingi bilioni 554.5 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya dharua iliyoathriwa na mvua za El- Nino na Kimbunga Hidaya ambapo kati ya mikataba hiyo yenye thamani ya Shilingi Bilioni 412 sawa na asilimia 74 inatekelezwa na wakandarasi wazawa.
Waziri Ulega ameeleza kuwa Serikali kupitia Wizara hiyo imeandaa mikakati ya kuwasaidia Wakandarasi wazawa na Washauri Elekezi ili waweze kunufaika kupitia miradi inayotolewa nchini na kuwataka watendaji wa Wizara kutoa ushirikiano na kuhakikisha wanatatua changamoto zinazowakwamisha wakandarasi wa ndani kupata miradi.
Ulega ameeleza kuwa Serikali inatambua mchango wa wakandarasi wa ndani kwani wamekuwa msaada mkubwa wakati wa urejeshaji wa mawasiliano ya barabara na madaraja mara baada ya miundombinu hiyo kuathiriwa na mvua za El-Nino na kimbunga Hidaya.
Kwa upande wake, Msajili wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), Mhandisi, Rhoben Nkori, ameipongeza Serikali kwa kuendelea kuwainua wakandarasi wageni kwani changamoto nyingi ambazo zimekuwa zikiwakabili wakandarasi hao zimeshafanyiwa kazi ikiwemo sheria ya ununuzi wa umma ya mwaka 2023 na kanuni zake za mwaka 2024 ambapo imetoa nafasi kwa wazawa kutekeleza miradi mikubwa zaidi hadi kufikia thamani ya Bilioni 50.
Akitoa neno la shukrani, Mkadiriaji Majenzi Samuel Marwa ameshauri Serikali kupitia CRB ihakikishe kuwa inafanya uhakiki wa kina kutambua kampuni za wazawa ili zabuni za miradi zinazotolewa ziwanufaishe wazawa husika na si vinginevyo.
Photo by:Admin, 2025-05-05 06:03:41 |
Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega ametoa siku 30 na kumtaka Mkandarasi Kampuni ya CHICO anayetekeleza ujenzi wa upanuzi wa barabara ya Nsalaga - Ifisi (km 29) kwa njia nne, jijini Mbeya kuongeza kasi ya ujenzi wa mradi huo ili uweze kukamilika na kupunguza msongamano wa magari katika jiji hilo.
Aidha, Waziri Ulega amemuagiza Mkandarasi huyo kufanya kazi usiku na mchana, kuongeza vifaa pamoja wafanyakazi ili kufanikisha mradi huo ukamilike haraka iwezekanavyo.
Ulega ametoa maelekezo hayo jijini Mbeya wakati alipokuwa akikagua maendeleo ya mradi huo na kutoridhishwa na hatua za utekelezaji wake ambao hadi sasa umefikia asilimia 25.
Ulega ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tayari imeshatoa malipo ya Shilingi Bilioni 35 kwa Mkandarasi huyo na matarajio yake ni kuona kupitia fedha hizo angalau kilometa kadhaa za lami zimekamilishwa kujengwa katika barabara hiyo.
“Serikali imeshatoa Bilioni 35 kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii kutoka Nsalaga hadi Ifisi, na fedha hizi Mkandarasi hajazifanyia kazi ipasavyo, Sasa basi Nimemuagiza Mkandarasi afanye kazi usiku na mchana na kuona mabadiliko ya haraka katika mradi huu”, amesisitiza Ulega.
Pia, ametoa maelekezo kwa Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Mbeya kumsimamia Mkandarasi kwa ukaribu ili hadi kufikia mwanzoni mwa Mwezi Juni mwaka huu Mkandarasi awe amekamilisha kilometa 10 za lami katika barabara hiyo na kuahidi kurudi tena kwa ajili ya kukagua maendeleo hayo.
Ulega amemuelekeza Meneja huyo wa TANROADS kuhakikisha ujenzi wa barabara hiyo unaenda sambamba na ufungaji wa taa za barabarani ili kuupendezesha mji wa Mbeya na kuimarisha masuala ya ulinzi na usalama wa wananchi wanaotumia barabara hiyo katika shughuli zao za kiuchumi za kila siku.
Vilevile, Ulega amepokea Ombi la Mbunge wa Mbeya Mjini na Spika wa Bunge la Tanzania, Dkt. Tulia Ackson la ujenzi wa kilometa tano za lami zinazoingia katika mitaa ya iiji la Mbeya na kuahidi kulifanyia kazi.
Kadhalika, Ulega amemuagiza Meneja wa TANROADS mkoa wa Mbeya kumsimamia Mkandarasi katika kuhakikisha kazi ndogondogo zinazofanywa na Mkandarasi zinatolewa kwa vijana wa Mkoa wa Mbeya ili kutoa fursa za ajira na vijana hao waweze kunufaika na matunda ya mradi.
kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini na Spika wa Bunge la Tanzania, Dkt. Tulia Ackson ameeleza kuwa wananchi wa Mbeya wamekuwa wakisubiri kwa hamu upanuzi wa barabara hiyo kukamilika ili kutatua changamoto za msongamano wa magari jijini humo.
Dkt. Tulia ameiomba Wizara ya Ujenzi kufanyia kazi mapendekezo yaliyoombwa katika barabara hiyo ya kuongezwa kwa barabara kilometa 3.5 kuanzia Ifisi hadi Songwe Airport na kilometa 5 kuanzia Nsalaga kuelekea Mlima Nyoka katika Bajeti mpya ya mwaka 2025/26 ili wananchi wa Mbeya kuendelea kunufaika na ujenzi wa mtandao wa barabara jijini humo.
Naye, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mbeya, Eng. Matari Masige ameeleza kuwa Mkandarasi anaendelea na ujenzi wa matabaka ya udongo G3, G7 na G15, ujenzi wa makalvati madogo na makubwa pamoja na ujenzi wa daraja la Nzovwe katika barabara hiyo.
Photo by:Admin, 2025-04-23 06:48:31 |